Nilipokuwa mfasiri, Kiswahili hakikuwa katika lugha zangu za kiutaalamu. Kwa hiyo, kama nimefanya makosa katika tafsiri hii hapa (ya karatasi yangu ya kizungu iliyotangulia), ambayo sijapitisha ikasahahishwe, tafadhali, naomba msinisulubishe. Maanake najaribu kama al-waatan wa kijiweni! Hata hivyo, nilijaribu kutafsiri hoja yangu kwa sababu njia bora ya kukuza lugha ni kuitumia lugha hiyo hiyo (uthibitisho wa ubora wa nyama ni kuitafuna hiyo nyama, au?)
1. Hoja yangu
Kwa nini, na kwa jinsi gani nchi au jumuhia ya mataifa kadhaa linapaswa kukienzi Kiswahili ili kije kuwa lugha ya Kiafrika na ya Kimataifa? Nauliza hivi maanake tunahitaji umakini wa kuondoa hali ya ukoloni didhi ya Afrika katika mikusanyiko ya kimataifa. Lugha ni kianzio cha nguvu Zaidi maanake inasimamia utamaduni na utu wetu, na ni chombo cha kuraisisha biashara kati yetu hapa Afrika. Kiswahili kinazungumzwa na watu takriban milioni 200 Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Maziwa Makuu, na kiko mbele ya Kihausa, kinachozungumzwa na watu milioni 80 katika ukanda wa Sudano-Sahel, yaani Sudan, Chad, Nigeria, Niger, Mali, Senegal, Guinea. Kwa hivyo Afrika inaweza kuunga mkono usambazaji wa Kiswahili, ili kucukuwa nafasi yetu duniani, bila utata, bila kuomba.
2. Sifa zangu zinaanzia wapi?
Miongoni mwa taaluma mbalimbali nilizokuwa nazo katika maisha yangu ya mfanyakazi wa umma, niliwahi kuwa mfasiri wa kujitegemea. Maana yake ni kwamba ukinikuta katika umati wa watu na nikimsikiliza mkalimani fulani, nitakuwa miongoni mwa wale watu ambao watatambua moja kwa moja kama mkalimani huyo anajua anachofanya, au kama anajichanganya tuu, kwa maana anatafsiri vibaya, anapotosha. Wazungu wanasema “lost in translation”.
Kiutaalamu, mitindo ya upanuzi wa lugha iko mitatu: (i) kutafsiri, (ii) ukalimani na (iii) Usahahishaji (usomaji sahihi). Mfasiri anachukua maandishi kutoka lugha moja hadi maandishi ya lugha nyingine. Mkalimani moja kwa moja anapaza sauti ya mtu mwingine katika hotuba. Kwa hiyo mkalimani anapashwa kuwa na kasi ya kuelewa na upokezi ambayo haitakiwi kwa mfasiri. Niongeze kwamba kuna aina mbili za wakalimani: wakalimani kwa mikutano ya umati, ambao huzungumza kwa vipindi baada ya mzungumzaji mkuu kutoa hoja na kuruhusu ubadilishaji wa lugha. Na mkalimani wa wakukimbizana na mzungumzaji mkuu, kwa kawaida huyu anatumika kwenye mikutano, ambapo mkalimani anazungumza wakati huo huo na mzungumzaji mkuu, kwa lugha nyingine. Kunakuwaga na viombo vinavyosaidia kuwasilisha hizo sauti ambavyoi pia viaruhusu wasikilizaji kuchagua lugha inayopendekezwa kupitia njia za michrophone. Mkalimani huyu kwa kawaida haonekani pamoja na mzungumzaji na anafanya kazi zake katika kibanda cha kujificha, na ni mtaalamu aliyejifunza kikamilifu.
Tafsiri ya kitaalamu inaenda sambamba na utaalamu wa tatu: kusahihisha. Kwa maana, msahihishaji ni mfasiri msomi anayekagua nyarakati zilizotafsiriwa kwa usahihi wa kisarufi, akimaanisha uadilifu na kushika vizuri mielekeo na misemo ya kitamaduni. Anahakikisha kuwa hakuna chochote katika lugha asilia kilichopotea katika utafsiri.
Mwishowe, wewe msomaji wangu ujuwe kuwa taaluma hizi zinalipwa sana. Huko nyuma mwaka wa 1987, kama mfasiri katika mikutano minne ya OAU, shirika tangulizi la AU, nilikuwa nalipwa dola 24 za Marekani kwa kila ukurasa niliotafsiri. Miaka 36 imepita, na tafsiri, kati ya taaluma hizo tatu, ndiyo ilikuwa inalipwa kidogo zaidi!
3. Kesi yenyewe
Lugha ya bara inayounganisha itakuwa chombo cha kidiplomasia muhimu sana katika kuinua sauti ya Bara la Africa kimataifa. Katika taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, ziko lugha sita ambazo ni rasmi: Kiingereza, Kifaransa, Kirusi, Kihispania, Kiarabu, Kichina. Maoni ya Kiafrika huwa yanapuuzwa na vyombo vya mawasiliano vinavyotawala anga ya kimataifa leo. Kama Afrika itapenda kusikilizwa, Kiswahili pekee ndiyo lugha yenye uwezo wa kupanuka na kuwa chombo cha kwanza mikononi ya bara la Africa.
Kiswahili ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya SADC na ya Umoja wa Afrika. Kwa kutokana na hoja ya kitaasisi na idadi ya watu, nahisi msingi na kesi zipo za kutosha kugeuza Kiswahili kuwa lugha ya msingi kwa Bara la Afrika.
Matamko na matakwa pekee hayawezi kufanya lugha iwe ya kimataifa. Taasisi za kitamaduni kama Taasisi ya Confucius, Alliance Française na British Council ndiyo yanasambaza lugha. Kusherehekea tu Siku ya Kimataifa ya Kiswahili iliyotangazwa na UNESCO ni kupendeza kwa kidiplomasia. Tunahitaji kuenda mbali zaidi, ili tuweze kuchukua nafasi yetu kwenye meza ya kimataifa na kushiriki katika kuunda kanuni mpya za ulimwengu, mahusiano, na biashara. Hiyo itairuhusu Afrika kuwasilisha ulimwenguni simulizi tofauti za kujenga, na kuvunja ukiritimba wa kitamaduni wa dhuluma na unyonyaji zinazotawala Bara la Afrika, kwa kupitia udhibiti wa mtiririko wa habari (na wa vichwa vyetu).
Kama lengo la muda mrefu, nchi za Afrika Kaskazini, Magharibi na Kusini mwa Afrika zinaweza kuthamini umuhimu wa kidiplomasia na kiutamaduni wa Kiswahili na jinsi hii lugha inajenga umoja. Tunahitaki sasa kuhamisha lugha hii kutoka somo la anayetaka hadi somo la kawaida shuleni. Itabidi Kiswahili kisaidie kukuza nafasi ya kiuchumi ya Afrika na uendeshaji wa diplomasia na mahusiano ya kimataifa.
4. Ufadhili
Nchi au Shirika la Kikanda linapaswa kuongoza huu mchakato. Chuo kikuu kingekuwa mahali muhimu pa kuendeleza kitaaluma, kiisimu na kifalsafa kwa mpango huu, kwa kuanzisha Taasisi ya Kimataifa ya Walimu, Wafasiri, Wakalimani na Wasahihishaji wa Kiswahili.
Taasisi hiyo ingehitaji kuanza na Shule ya Lugha za Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiswahili na Kirusi, kwa nia ya kukifanya Kiswahili kuingia katika nyanja za kitaaluma za (a) utafsiri, (b) ukalimani na (c) usahihishaji. Ni muhimu kusaidia upanuzi wa uwezo uliopo wa utafiti wa kitaifa katika [a] Vyuo Vikuu vilivyochaguliwa, na huo msaada ni matarajio halali. Jitihada hii ya kitaaluma inaweza kujifunza kutoka kwa Taasisi zilizopo kama Chartered Institue of Linguistics duniani (Uingereza, Kanada, Marekani, Afrika Kusini na kadhalika) na kuwa Chartered ya kujisimamia yenyewe hapo baadaye.
Kiini cha Taasisi za Wafadhili: hakuna kinachosonga mbele bila kusukumwa. Hivyo, vinahitajika:
Msaada wa kidiplomasia na wa kishirika: hii ndiyo nguzo ya kuendeleza mpango.
Msaada wa Kiakademia: [a] Chuo/vyuo Kikuu[vi], pamoja na uimarishaji wa kitaasisi utakaohitajika.
Msaada wa kisiasa: Umoja wa Afrika, EAC, SADC
Msaada wa Kifedha: Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mfuko wa Kimataifa wa Elimu, n.k.
Mkakati wa Kitaaluma: Utafiti na Maendeleo ya Lugha
Mafunzo ya Maprofesa wa Kiswahili,
Kuhitimu kamili, ikiwezekana katika kiwango cha MA, cha Usahihishaji wa Kiswahili,
Mahafali kamili, ikiwezekana katika kiwango cha BA, ya Wakalimani wa Kiswahili,
Kuhitimu kamili, ikiwezekana katika kiwango cha BA, kwa wafasiri wa Kiswahili,
Mahafali yatakuwa ya ukalimani, tafsiri na usahihishaji wa Kiswahili kwa lugha mbili na kwa lugha nyingi katika lugha sita za Umoja wa Mataifa. Taaluma hizi lazima ziwe wazi kwa nchi zote za Afrika.
Kukipeleka Kiswahili kuwa lugha ya Kimataifa (italazimika kuwa ratiba ya programu ya miaka mingi: kuanzisha, kuwasilisha, kufanya ikubalike kwenye makongamano)
Awamu ya kwanza: kuifanyia kampeni Kiswahili Kanda la Afrika.
Awamu ya Pili: Msaada wa kitaasisi kwa [a] Vyuo Vikuu kwa ajili ya kuimarisha Ufundishaji wa Kiswahili na kwa taaluma ya uwezo wa Tafsiri, Ukalimani na Usahihishaji.
Awamu ya Tatu: Kuimarishwa kwa taasisi za bara ambazo tayari zinatumia Kiswahili (AU, EAC, SADC): kuwekeza zaidi katika kuboresha na kuwapa taaluma wakalimani, wafasiri na wasahihishaji wao.
Awamu ya Nne: Miradi ya Majaribio ya Upanuzi: kupeleka Kiswahili katika taasisi za kimataifa zenye makao makuu yake barani Afrika: United Nations Economic Commission for Africa (ECA- Addis Ababa), UNEP na UNHABITAT (Nairobi). Hii itatupeleka
Awamu ya Tano: Kuingiza Kiswahili katika Sekretarieti za Umoja wa Mataifa New York na Geneva. Upanuzi wa taratibu katika Programs and Funds tofauti za mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Ingawaje nchi moja inaweza kudai umilisi wa Kiswahili kitaaluma, kitamaduni na kidemografia, na inaweza kuanzisha au kuteuliwa kufanya mradi huu, itakuwa mtazamo wa kidiplomasia kushirikiana na serikali nyingine zinazohusika katika Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi, ambako Kiswahili ni lugha rasmi. Kusimamia mradi huu kunahitaji uongozi wa pamoja katika shughuli, kifedha na kitaasisi.
Niseme zaidi kwa kusisitiza: huu hauwezi kuwa mchakato wa muda mfupi na nchi/taasisi yoyote inayoipigia debe haiwezi kuiweka chini ya siasa za (ma)taifa (ya)inayoendesha hii programu, yaani kuangalia awamu za uchaguzi au za vyeo vya kisiasa. Huu mchakato unapendekezwa kama huduma inayotolewa kwa niaba ya Bara zima la Afrika.
5. Usimamizi
Hili ni jukumu kubwa kwa niaba ya Bara zima na nchi/shirika lolote la Kikanda linaloongoza katika mradi huu linaweza tu kuutekeleza kupitia ruzuku. Inapendekezwa kuwa ruzuku hizo zitafutwe hasa miongoni mwa taasisi za fedha za Afrika, kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Hivi ni vita vya kitamaduni, si mazungumzo ya kitamaduni mkiwa mmekiti na kunywa chai na kupiga adithi, ambapo mpatanishi wako angetarajiwa kutangaza "acha Kiswahili kiwe lugha ya kidiplomasia ya kimataifa pia!" Ukitarajia kuingia tu kwenye chumba cha mikutano na kuanza kuongea Kiswahili kwa sababu kuna mtu alitangaza, angalia tena kama hotuba yako haijachukuliwa na upepo. Ulimwengu siyo zawadi kwa Afrika. Wamexzoea kuonma bara la Afrika kama mali yao.
6. Swali kwa wasomaji wangu wote, kwa viongozi wetu
Kwa nini tunayo biblia ya Kikristo (katika matoleo yake yote kadhaa) iliyotafsiriwa kwa Kiswahili, Kinyanja, Kishona na lugha nyingi za Kiafrika, lakini hatujatafsiri katika lugha yetu yoyote vitabu vya hisabati, fizikia, jiografia, sayansi, kemia, trigonometry au biolojia? Je, tutawezaje kujenga daraja bila kukimbilia Wachina ikiwa mwanafunzi wetu haelewi trigonometry kwa Kiingereza? Wote tunajua historia ya kikoloni ya Biblia; Naweza kutoa ili swali kwa kuigeuza: wakati gani tunapaswa kuanza kutumia lugha za Kiafrika ili kukuza utafiti wa kitaaluma na ujuzi wa kisayansi? Wachina vitabu vyao vimeandikwa ki Mandarin, Wajapani katika lugha yao, Wahindi katika lugha zao. Kwa nini tutashangaa kwamba hatupate maendeleo yoyote ya kiteknolojia wakati tumejiwekea kikomo na kujifunga na lugha za Kifaransa, Kireno na Kiingereza? Je, hatuwezi kuwa na akili za kutosha ili tuichukue changamoto hizi kama juhudi za bara letu?
Je, baada ya Kiswahili hatuwezi kujisogeza Zaidi na Kihaussa? Na… na…?
Kuna msemo wa Kireno: Quem põe o guizo ao gato? (Nani atamsogea paka na kumpachikia kengele shingoni?)
Antonio Jose Canhandula, Julai 2023
Comments